Maandiko yote ni kutoka tafsiri ya NKJV isipokuwa pale yatakapoelekezwa vinginevyo.
MANENO MUHIMU: Neema, mwenye neema, kibali, kupokelewa kama mwana, umwana, kusudi lililoko nyuma ya neema.
Muhtasari: Je, Mungu ni Mungu wa Israeli tu—au wa ulimwengu mzima? Neema/kibali cha Mungu ni kwa ajili ya nani? Na KWA NINI Mungu alikuja na neema na kibali chake cha thamani kwetu? Lengo lake la mwisho lilikuwa nini? Ikiwa wokovu si kwa matendo, basi kutii kwa Mungu kuna nafasi gani, ikiwa kuna nafasi yoyote? Lakini tunawajua baadhi ya watu waliofanya maovu yasiyosemekana. Je, neema ya Mungu itaweza kufunika dhambi mbaya kabisa, au kuna baadhi ya watu walio nje kabisa ya ukombozi na kuokolewa? Inakuwaje pale watu waliopata kuzaliwa upya/kubadilishwa na waliopokea Roho Mtakatifu wa Mungu wanapotenda dhambi? Je, Mungu bado anakupenda unapofanya dhambi? Haya na mengine mengi yatajadiliwa katika mafundisho haya.
** *** ************************ ********************* *****************
Habari zenu wote. Ninapendekeza mtazame video hii na pia mchapishe maelezo haya mkiendelea kufuatilia kwa sababu nitatumia maandiko mengi sana. Kuna mambo zaidi katika video.
Andiko kuu kuhusu kibali cha Mungu kilichojaa neema, linapatikana katika Waefeso 2, likisomwa na Scott Doucet, msimamizi wetu wa tovuti. (Yeye na mkewe Brandie wanafanya kazi kwa bidii kuhakikisha video hizi zote zinapatikana.)
Waefeso 2:8-10 (SUV)
“Kwa maana mmeokolewa kwa NEEMA kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni KIPAWA cha Mungu;
9 WALA si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.
10 Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.”
Baada ya kutoa mahubiri yangu ya mwisho nikieleza kuhusu neema ya ajabu ya Mungu ya kuokoa, mtu mmoja alitoa maoni akijaribu kupinga ujumbe wa Waefeso 2:8-9, kuwa tumeokolewa kwa neema, wala si kwa matendo yetu, ili mtu yeyote asije akajisifu. Basi akanukuu Warumi 2:13 -- “Kwa sababu sio wale wasikiao sheria ndio walio waadilifu mbele za Mungu, bali ni wale waishikao sheria watakaohesabiwa haki.” Kwa maneno mengine, alimaanisha kwamba hatutaokolewa kama hatufanyi jambo fulani; yaani kama hatutakuwa watendaji wa sheria.
Lakini ni kweli, wewe na mimi tungehesabiwa kuwa wenye haki – tumehesabiwa haki – IWAPO tungezitii sheria za Mungu kikamilifu na kuendelea kuzitii kikamilifu bila kukosea hata mara moja. Kama ingekuwa hivyo, tusingemhitaji Mwokozi wala neema yake! (Wagalatia 2:21. Hilo ndilo kusudi la Warumi 2. Lakini endelea kusoma, na katika Warumi 3 tunaambiwa—Lakini jamani, hakuna aliyeshika sheria kikamilifu (Warumi 3:10-11). HAKUNA HATA MMOJA, isipokuwa Kristo tu. Ndiyo maana tunasoma kile kinachoonekana kama kinyume na Warumi 2:13:
Warumi 3:20
“Kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria.”
Nadhani kibali cha ajabu cha Mungu kwa wale wanaokipokea kinaeleweka vibaya sana. Tafadhali hakikisha umesikiliza kwanza mahubiri yangu ya awali kuhusu Neema ya Mungu Iokoayo. Mahubiri hayo yataweka msingi ambao sitauzungumzia sana leo isipokuwa kwa kukumbusha kidogo. Kuna mengi zaidi ya kusema kuhusu kibali cha Mungu kilichojaa neema.
Warumi 3:20 haipingani na Warumi 2:13. Bali inaeleza kuwa kuwa mtendaji mkamilifu wa sheria ni jambo kubwa, ikiwa utaweza kumpata mtu anayezitii kikamilifu sheria zote na kwa hiyo hahitaji neema! Lakini kwa kuwa hakuna aliyefanya hivyo, neema ya Mungu inahitajika kwa kila mmoja wetu. Neema ya Mungu ni KIPAWA cha bure cha kibali kisichostahiliwa. Si kitu tunachoweza kukifanyia kazi au kukipata kwa matendo (Warumi 11:6-7). Matendo ni kwa ajili ya THAWABU katika Ufalme—lakini hayatuokoi.
Ndiyo maana tunahitaji kibali cha bure cha Mungu juu yetu kwa sababu wote wamefanya dhambi, na wote wanaendelea kufanya dhambi japo kwa kiwango kidogo, hata baada ya kupokea Roho wa Mungu, kama Paulo anavyosema katika Warumi 7. Kwa hiyo neema ya Mungu isiyostahiliwa ndiyo inayotuokoa. Natumaini wewe umeona kuwa unahitaji neema ya Mungu ya kuokoa – hasa unapojilinganisha kidogo tu na utakatifu mkamilifu wa Mungu ukilinganisha na wako.
Neema ni KWA AJILI YA ULIMWENGU WOTE
Sehemu hii ya pili ya mahubiri kuhusu Kuishi katika FURAHA ya Neema ya Mungu -- si kwa ajili ya kundi lolote la kanisa fulani, bali ni kwa ajili ya makanisa yote na dini zote.
Mungu hakumtuma mwana wake kuishi na kufa na kufufuka kwa ajili ya Wayahudi tu, au kwa ajili ya wale walioko sasa katika Ukristo, au kwa ulimwengu wa Magharibi tu. La hasha! Yesu alikubali wito wake kuwa “Mwokozi wa ULIMWENGU mzima” (1 Yohana 2:1-2).
Kwa hiyo mahubiri haya ni pia kwa ajili yenu Wahindu, Waislamu, Wabudha, wasioamini Mungu, wale wa dini ya Kiyahudi, Wakatoliki, Waprotestanti, wanaoshika sabato, kwa kifupi, kwa kila mtu. Mungu alimtuma mwana wake “ili awe MWOKOZI wa ULIMWENGU”— (1 Yohana 4:14).
Ndio maana nawaona watu wote, bila kujali mwenendo wao au dini yao, kama kaka na dada zangu—ambao bado hawajajua ukweli huu! TUNAPOANZA kuelewa kusudi la Mungu, na neema ya Mungu, hakika tunaweza kuanza kuishi Maisha mapya ya Kiumbe kipya kwa FURAHA!
Wokovu kwa njia ya neema ya Mungu ni kwa kila mtu anayeitika mwito wa Mungu kwake, akiwa kokote ulimwenguni. Mara tu tunapoamini kweli kwamba Mungu anafurahia kuwa na WEWE katika familia yake, tunaanza kujifunza kuishi katika furaha ya neema ya Mungu inayookoa.
1 Yohana 2:1-2 (NIV)
“Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki;
2 Naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ULIMWENGU WOTE pia.”
Mungu wangu anawakukaribisha kutoka sehemu zote za ulimwengu kuchunguza neema ya kweli ya wokovu kutoka kwa Mungu aliye hai, na kuishi katika KIBALI chake licha ya maovu yote uliyowahi kuyafanya huko nyuma au hata sasa, au hata kama dunia yako imeharibika kiasi gani.
Haijalishi kama wewe ni Mkristo, Mbuddha, Mhindu, wa dini ya Kiyahudi, ulikuwa Mwislamu, Mkatoliki – au chochote kile… Muite leo na uingie katika NJIA yake, NJIA ya wokovu kwa kibali na neema ya Mungu kama ilivyofunuliwa katika Neno lake.
Nina uhakika, kwa sababu ya kibali hiki cha ajabu kutoka kwa Mungu wetu, kwamba nitakuwa katika Ufalme wake na nitapata uzima wa milele. Natumaini kuwa nitawaona wengi wenu huko pia – hata kama bado leo hii wewe si Mkristo wa kweli wa kuishi kwa matendo, ninatumaini UTAMWAMINI Yesu Kristo, na… ningefurahi sana kukutana na wewe unayesikia ujumbe huu siku moja katika Ufalme wa Mungu.
Somo hili ni gumu kulitimiza au kulikamilisha kabisa. Tafadhali hakikisha UMEANGALIA sehemu ya (1) kwanza kwa ajili ya msingi.
Karibu kwenye Light on the Rock. Mimi ni Philip Shields, mwenyeji, na mwanzilishi wa tovuti hii ya bure ambapo lengo letu ni kuwasaidia watu kuwa na uhusiano wa karibu zaidi na Mungu, kumpenda Mungu kwa moyo wote, na kuwapenda watu – hata maadui wetu – kwa upendo wa dhati zaidi. Kumbuka kutembelea sehemu ya maandiko mafupi, blogu, na mahubiri yetu ambayo yatakuwa mchanganyiko wa video na sauti, pamoja na mengine MAPYA.
Kwa sasa tuna watu 5-6 tu – ndivyo ilivyo! – wanaosaidia kazi hii ya kumleta Kristo kwa watu, na tunashukuru kwa msaada wenu. Michango hiyo inasaidia vituo vya watoto yatima maskini na makanisa nchini Kenya, na pia kuwasaidia wajane hapa Marekani mara kwa mara.
Basi “lengo la mwisho ni nini” - Kwa nini Mungu anatupa kibali hiki cha ajabu? Anajaribu kufanikisha nini kupitia kibali chake?
KUSUDI la Neema ya Kweli na Kibali cha Mungu
Kimsingi, naamini hili ndilo jambo kuu: Mungu aliye Juu Zaidi – tunayemwita “BABA” – anataka kuwa na uhusiano wa kifamilia wa upendo na watoto wake mwenyewe. Mungu tayari ana watoto sasa ("Je sisi ni Watoto wa Mungu..." – 1 Yohana 3:1-3; Warumi 8:14-17).
Neno, ambaye alikuja katika mwili kama Yesu Kristo (au Yeshua, jina lake la Kiebrania) alikuwa "MZALIWA WA KWANZA miongoni mwa ndugu WENGI" (Warumi 8:29).
Sisi watoto wengine wa Mungu ni kaka na dada wa Kristo. Yeye ndiye mtoto wa kwanza wa Mungu. Yeshua mkamilifu "haoni haya kutuita ndugu zake" (Waebrania 2:10-11). Kuhusu Yeshua, Maandiko yanasema:
Yohana 1:10-13
"Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. 11 Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea.
12 Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; 13 waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu."
Mtoto wa MUNGU. Kuzaliwa na MUNGU. Tafakari hilo! Kwa hiyo wewe uliitwa na Mungu, ambaye alikuongoza kwa wema wake kuufikia toba (Warumi 2:4) – na naamini Mungu alikuwa akikutenda kazi na kukuchagua tangu utotoni mwako, na kwa baadhi ya watu hata kabla hawajazaliwa (Waefeso 1:4-6). Kisha alikusukuma, kama alivyomfanyia Sauli/Paulo (Matendo 9:3-5) ili uitikie mwito wake!
Katika kibali cha Mungu kilichojaa neema, anatupa Roho wake ambaye hutuzalia katika familia yake – "kilichozaliwa kwa Roho ni roho" (Yohana 3:5-8) na Mungu ana watoto wengi. Mara tunapopokea Roho Mtakatifu wa Mungu, SISI NI WA MUNGU na wa Kristo. Haleluya! (Yohana 17:9-10; Warumi 14:8; 2 Wakorintho 10:7)
Warumi 8:29 (pia soma Waebrania 2:10-11)
"Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi."
Tafakari hilo vizuri. "KUZALIWA NA MUNGU." Hilo ndilo lengo kuu la yote haya. Kumwamini Yesu Kristo kunamaanisha kujisalimisha kabisa kwake kama Mkuu wetu na BWANA, na kuamini kuwa alifufuka kutoka kwa wafu ili kuishi kwa ajili yetu na kuwa Mfalme wa Ufalme wa Milenia ujao. Mungu Baba amempa mwana wake mzaliwa wa kwanza vitu vyote – na atavishiriki na wale watakaokuwa katika ufufuo wa kwanza kama warithi pamoja naye wa mambo yote (Warumi 8:14-17). LAKINI pia huenda tukapaswa kuteseka, kwa maana kupita katika mateso kwa amani na imani ni njia mojawapo ya kufanywa wakamilifu (Waebrania 2:10-12).
Yohana 1:14
"Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.
Mwana wa Mungu alikuja kulipa deni AMBALO hakuwahi kulidaiwa, kwa sababu SISI tulikuwa na deni AMBALO hatukuwa na uwezo wa kulipa.
Kumbuka kutoka kwenye mahubiri ya sehemu ya kwanza, kwamba “neema” katika Agano Jipya inamaanisha KIBALI cha Mungu, upendo wake, baraka zake, kukukubali wewe – pamoja na msamaha na kuachiliwa kwa dhambi zetu zote.
Hii ndiyo SABABU Yesu aliweza kuwa rafiki wa wenye dhambi. Aliwaona kama sehemu ya familia ya Mungu hapo baadaye pia. Alitaka nao waokolewe. Sisi tunahitaji kuwa na mtazamo huo huo wa Kristo (Wafilipi 2:5).
Kwa hiyo, kwa wote wanaoamini katika maisha, kazi, na ufufuo wa Yeshua Masiya, Mungu anawapa haki ya kuzaliwa na Mungu. Usimdharau mtu yeyote! Kuwa rafiki mwema kwa majirani zako na wenzako wa kazi. Pengine Mungu atakutumia kuwapelekea Injili ya Ufalme wa Kristo na kibali chake kilichojaa neema.
Kwa hiyo MAANA ya yote haya kuhusu “Charis” (neno la Kigiriki kwa ajili ya "neema") ni kushirikiana na wanadamu ili—kila mmoja kwa wakati wake uliopangwa—tuweze kuwa watoto wa Mungu wa kweli, waliokamilika katika roho, kama inavyoelezwa vizuri sana katika 1 Wakorintho 15 na 2 Wakorintho 5.
Mungu alihitaji kuwa na watoto watakatifu, waliotengwa kwa ajili yake, ambao wameukataa uongo wa Shetani na wamechagua Mungu na NJIA YAKE—siyo yule nyoka aliyetoa manung’uniko na uongo wake bustanini. Watoto ambao wanapigana dhidi ya dhambi inayotuzunguka kwa urahisi sana. Lakini Roho iko tayari, kama Yesu alivyosema, lakini mwili ni dhaifu (Marko 14:38). Kwa hiyo tunaishia kutenda dhambi bado, hata baada ya kupokea Roho Mtakatifu wa Mungu.
Angalia pia mahubiri yetu ya sehemu 3 ya "Hatima Yako ya Kushangaza". Hii ni Sehemu ya 1. Septemba 2017. Light on the Rock – Hatima Yako ya Kushangaza! Sehemu ya 1 – na Philip Shields.
Bila shaka tunahitaji kibali cha Mungu kilichojaa neema (charis – inatamkwa “HAR-is”) – kwa sababu sote tumetenda dhambi na tumestahili adhabu ya kifo, na bado mara kwa mara tunatenda dhambi.
Warumi 6:23
“Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali KARAMA ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.”
Kwa hiyo Mungu alitupatia wokovu kwa NEEMA kupitia imani, nasi tukaukubali. Uzima wa milele, wokovu, msamaha wa dhambi zetu zote, kupokea UPENDO wa Mungu—vyote hivi ni KIPAWA kutoka kwa Baba mkamilifu. Hakuna kitu unaweza kufanya au ambacho Mungu anataka ukifanye kitakachomfanya Mungu akuokoe zaidi au akupe uzima wa milele zaidi. Wote tunaokolewa na kupata uzima wa milele pale tunapoamini.
IMANI YA KWELI INAAMBATANA NA KUMTII MUNGU, HII NDIYO MAISHA YETU MAPYA
Kumwamini Yeshua kwa kweli kunamaanisha kwamba Yeye ni Bwana na Mwalimu wetu. Inamaanisha tumeamua KUMTII na kuacha njia ya Shetani. Hatuwezi kula mezani pa Bwana na pia mezani pa mashetani kwa wakati mmoja (1 Wakorintho 10:21). Ndiyo maana mimi sishiriki katika tamaduni na sikukuu za kipagani.
Waebrania 5:8-9
“na, ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; 9 naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote WANAOMTII.”
Kumtii Mungu ni uthibitisho kwamba umejisalimisha kwake kwa kweli na una IMANI katika kile anachotuambia tufanye na tuwe. Kile tunachoamini kwa kweli huonekana kwa matendo yetu. Kwa mfano, Ibrahimu ALIMWAMINI Mungu, na kwa hiyo alikuwa tayari kumtoa sadaka mwanawe Isaka, akijua Mungu hawezi kusema uongo na alikuwa ameahidi uzao kupitia Isaka. Hivyo basi, imani yetu na kuamini kwetu kunamaanisha tunatii. Kutiii siyo “matendo kwa ajili ya wokovu”—bali ni kujisalimisha kabisa na kuamini kwa dhati katika Mungu.
Utiifu wako, hata matendo yako mema, ni USHUHUDA na uthibitisho kwamba umepokea neema ya wokovu. Kumbuka Waefeso 2:8-10 inasema tumeumbwa kwa ajili ya matendo mema.
Waebrania 3:18-19
“Tena ni akina nani aliowaapia ya kwamba hawataingia katika raha yake, ila wale WALIOASI?
19 Basi twaona ya kuwa hawakuweza kuingia kwa sababu ya KUTOKUAMINI kwao.”
Utii wetu ni ushahidi wa imani, uaminifu, na tumaini letu katika Mungu. Kutokutii hutokea kwa sababu ya kutokuamini (au udhaifu), kama tulivyomaliza kusoma.
Kwa hiyo neema ya kweli ya Mungu na kibali chake huja kwa wale wanaokubali mwito wake wa kumwamini Kristo kwa dhati, kumtii, na kujisalimisha kwake… Kisha tunabatizwa na kupokea Roho Mtakatifu wa Mungu kwa kuwekewa mikono na wahudumu wake (Matendo 2:38).
(Kuna maandiko mengine mengi ya kujifunza kuhusu haja ya utiifu – Matendo 6:7; Warumi 15:18-19; 16:26; 2 Wakorintho 10:4-6, na mengine mengi.) Na je, Yeshua hakuwambia wanafunzi wake wafundishe watu kuyashika yote aliyowaamuru? (Mathayo 28:18-20). Na Roho Mtakatifu hupewa wale wanaotii (Matendo 5:32). TUNATII kwa sababu tunataka.
Maisha ya utii ndani yetu ni kwa sababu tunamfuata Yeshua; ANAFANYA kazi sasa ndani yetu, akiishi maisha ya utii na haki. Yule “mimi wa zamani” siye tena anayeishi, bali Kristo anaishi ndani yetu, na tunaishi kwa imani ndani yake na kwa imani yake (Wagalatia 2:20). Tunapomfuata kwa utii, “tunatembea kama yeye alivyotembea” (1 Yohana 2:6).
Changamoto yetu huja wakati tunatambua hatutii kila wakati, bali tunaanguka, tunateleza katika dhambi—lakini bado TUNAAMINI kwa Kristo na Baba yetu. Dhambi za namna hiyo pale tunapotubu kila wakati zinafunikwa, kama nilivyoeleza, na hatuhukumiwi, hatukatwi, hatutengwi, wala hatukataliwi, wala hatupungukiwi na upendo wa Mungu kwa ajili ya dhambi hizo, hasa sasa kama mtoto wa Mungu.
NEEMA YA MUNGU INAFUNIKA HATA DHAMBI MBAYA KABISA
Haijalishi maisha yako yamekuwa ya aina gani, au dhambi zako zimekuwa gani, Neno la Mungu linasema kwamba kibali chake kilichojaa neema kinatosha kabisa kukufunika, kukusamehe, kukupenda, na kukukubali katika familia ya Mungu. Uuaaji, ubakaji, kuwadhulumu watoto, kuchoma moto mali ya watu, kusema uongo, kuiba—kutamani. Au zile dhambi mbaya sana za KIBURI na kujiona mwenye haki, kwa sababu hujioni kuwa mbaya kiasi hicho… au hujioni kama wengine walivyo wabaya.
Lakini kumbuka, haki yetu sisi wenyewe ni kama nguo ya uchafu machoni pa Mungu, kumbuka (Isaya 64:6). Basi, haya yote yanafunikwa pia na neema yake—ikiwa utamwamini Yesu Kristo kwa moyo wako wote na nafsi yako yote, na kuukubali mwito wa upendo wa Mungu Baba kwako.
Tafsiri moja ya Warumi 5:20 inasema kwamba pale dhambi ilipozidi, 'neema ilizidi sana zaidi.' Hakuna mtu anayeweza kutenda dhambi kupita uwezo wa neema ya Mungu kukuosha na kukutakasa.
Warumi 5:20-21
“Lakini sheria iliingia ili kosa lile liwe kubwa sana; na dhambi ilipozidi, neema ilikuwa nyingi ZAIDI; 21 ili kwamba, kama vile dhambi ilivyotawala katika mauti, vivyo hivyo kwa njia ya haki neema itawale hata uzima wa milele kwa Yesu Kristo Bwana wetu.”
Hakuna dhambi wala mwenye dhambi aliye mbaya kupita neema ya Mungu. Hata wale watu wabaya kabisa unaoweza kuwaza kuwahusu, iwapo Mungu aliwaita watubu, na kweli wakatubu—dhambi zao zinaweza kusafishwa kwa damu ya Kristo, na wanaweza kukombolewa na kupatanishwa na Mungu. Ndiyo, hata wabaya kabisa. Hakika Mungu anaweza kukufunika. (Isipokuwa: “dhambi isiyosameheka”—wale wanaokataa kwa kujua na kwa makusudi toleo la Mungu na kazi ya Roho Mtakatifu waliyopewa).
Neema ya Mungu ina nguvu kubwa sana kiasi kwamba Paulo alisema MOJA ya maelezo ya Injili yake ni “Injili ya Neema ya Mungu” (Matendo 20:24). Natumaini kwamba kusanyiko au kanisa lako linafundisha Injili hiyo kwa jina hilo!
MWANA WA MUNGU, KWA NEEMA YA KWELI, NDIYE ANAYETUBADILISHA
Kibali cha Mungu kilichojaa neema kinapaswa kutubadilisha tunapokwenda sambamba nacho, sambamba na Mungu. Na hiyo inapaswa kutujaza FURAHA ya wokovu wake. (Katika video tunajadili kuhusu Mfalme Daudi katika sala ya Zaburi ya 51—ambayo ilianza kwa huzuni na majonzi, lakini ikaishia kwa furaha na amani).
Kumbukumbu fupi ya baadhi ya vipengele vya mahubiri ya mwisho:
- Tulionesha Warumi 8:1-4, jinsi ambavyo baada ya Paulo kukiri kuwa aliendelea kujikwaa katika dhambi, haukumuwi tena sasa tunapotenda dhambi kama watoto wa Mungu! Kama watoto wa Mungu, hatuhukumiwi tena tunapoteleza katika dhambi. Tafadhali soma mwenyewe Warumi 8:1-4!
Kama Rafiki mzuri anavyosema: “Mungu alitangaza mwisho wa utawala wa dhambi juu yetu kwa kutupatia Mwana wake kuwa dhabihu ya dhambi zetu. Warumi 8:2-4 inasema wazi kabisa kwamba matakwa ya sheria ya Mungu yametimizwa kikamilifu KWA AJILI YETU, sisi tunaotembea kwa Roho na si kwa asili ya mwili.”
Wengi wenu mnaweza kuwa mnaona aibu au kiburi kupokea kitu chochote bure. Au mnaona aibu kukubali kile ambacho Mtu Mwingine amekufanyia, kama vile kutimiza kikamilifu na kutii sheria ya Mungu kwa niaba yako. Kristo amelipa deni lako—maana mshahara wa dhambi ni mauti. Yeye alitimiza sheria kikamilifu—na sasa anakupa zawadi ya kukuvika haki YAKE mwenyewe (Sikiliza mahubiri yangu kuhusu "Ukamilifu wa Mungu Kwa Ajili Yetu").
Hili ni MUHIMU SANA:
- Yeshua anakuja kuishi ndani yetu, na ni MAISHA YAKE yanayopaswa kuwa HAI ndani yetu, na tunapaswa kuwa karibu naye kiasi cha KUSIKILIZA na KUMFUATA. Yeye ataishi ndani yako kama alivyokuwa akiishi duniani: kwa utii. Lakini ni kazi yake, ni haki yake. Soma Wakolosai 1:28-29. Paulo alifanya kazi pamoja nao ili awasilishe kila mtu mkamilifu katika Kristo.
Wakolosai 1:28b-29
“…tupate kumleta kila mtu mkamilifu katika Kristo Yesu.
29 Nami najitaabisha kwa neno lilo hilo, nikijitahidi kwa kadiri ya kutenda kazi KWAKE atendaye kazi ndani yangu kwa nguvu.”
Ninaomba sana kwamba ningeliweza kusema kwa dhati kuwa najitahidi kuruhusu kazi ya Kristo ifanye kazi kwa nguvu ndani yangu. Hilo lingemaanisha kwamba kwa kweli namtafuta, namsikiliza, namtii, na namfuata. Baba, nisaidie kufanya hivyo.
Ndiyo, tunapaswa kupigana dhidi ya dhambi, tunapaswa kuihimili dhambi, tunapaswa kutubu tunapotenda dhambi, lakini kuna mengi yamebadilika sasa kwako na kwangu ikiwa tunaye Roho wa Mungu. Tuna asili ya "utu wa kale" aliyesulubiwa pamoja na Kristo, lakini njia ya kale—“mwili”—bado imo ndani yetu. Lakini siyo hiyo Mungu anayoiangalia (Warumi 8:8-9). Wakati tunapambana dhidi ya dhambi inayotuzingira kwa urahisi, hatutawahi kuishinda kabisa, hata kwa kuwa na Roho Mtakatifu wa Mungu, kama Paulo alivyokiri katika Warumi 7.
Nataka kukumbusha mambo ambayo wengine wanapata ugumu sana kuyakubali, na hivyo kukosa FURAHA ya neema ya Mungu. Kwa neema:
- Adhabu yetu ya mauti kwa nyakati zote sasa imelipwa ndani ya Kristo.
- Kristo alikufa mara moja tu kwa ajili ya wenye dhambi. Kitabu cha Waebrania kinasema hivyo mara kadhaa. Hatuingii tena chini ya hukumu ya mauti. Wale watakaoshiriki ufufuo wa kwanza hawapaswi kuogopa "mauti ya pili" (Ufunuo 20:6). Hilo limekwisha, limeamuliwa—hata pamoja na kujikwaa kwetu! Tumepita kutoka mautini kwenda uzimani! (Yohana 5:24)
- Tunapokea kipawa cha uzima wa milele kilichothibitishwa kwa kupakwa mafuta kwa Roho Mtakatifu (2 Wakorintho 1:21), mradi tu tudumu katika njia yake (Waefeso 1:13-14). Mungu pia ameahidi kukamilisha alichoanza (Wafilipi 1:6)—na kwa baadhi yetu, hilo linaweza kujumuisha majaribu makali, labda hata kihalisia, na hata mauaji, ikiwa hilo ndilo litakaloturudisha kwenye njia sahihi.
Kwa hiyo SIFUNDISHI maisha ya uasherati au anasa kama ilivyoonywa katika Yuda 4, SAWA???? Lakini kuzaliwa kwa mbegu ya Mungu, yaani ROHO wake, kama nilivyoeleza katika sehemu ya kwanza, ndicho kithibitisho bora zaidi kwamba Mungu atakamilisha kile alichoanza. Mungu hahusiki na “kuavya mimba kiroho! Mungu amesema hatampoteza hata mmoja aliye mkononi mwake. "Hakuna mtu" inamaanisha hata wewe utakuwa huko, ndani ya Ufalme wa Mungu.
Maandiko yako wazi: Lakini ikiwa utaendelea kuishi maisha ya dhambi kama mtindo wa maisha—hata baada ya kudai una imani katika Yeshua—UTAKUFA. (1 Wakorintho 9:6-9; Warumi 8:12-14; Waefeso 5:3-8; Wagalatia 5:19-21). Tunapaswa kuwa watiifu kadri ya uwezo wetu kwa msaada wa Roho wa Mungu.
IMANI, kwa hakika, mara nyingi huambatana na utii (Waebrania 3:18-19).
Waisraeli watu wazima wenye umri wa miaka 20+, hawakuingia katika nchi ya ahadi kwa sababu ya kutokuamini kulikosababisha kutotii mara kwa mara.
Ninaamini sisi SOTE bado tunayo dhambi tunazotenda mara kwa mara. Labda si kama mtindo wa maisha, bali ni kujikwaa—iwe ni kula kupita kiasi, kukasirika kupita kiasi, kuangalia ponografia mtandaoni, kulewa kupita kiasi wakati mwingine, kusingizia watu, kujihisi kuwa dhambi zako ni bora zaidi kuliko yule mtu usiyetaka hata kukaa naye, kujiona mwenye haki, kiburi, kutongoza hovyo, n.k.
Wale wanaoshinda, hao watapata THAWABU KUBWA zaidi. Wale wasioshinda sana, watapata thawabu ndogo zaidi, lakini WATAOKOLEWA. Mambo yote yanahusu imani katika Yesu na kama dhambi zetu ni maanguko ya hapa na pale au ni mtindo wa maisha!
TUSIRUDIE: mfano wa yule mwenye dhambi ya uasherati katika 1 Wakorintho 5. Alikabidhiwa kwa Shetani kwa maangamizo ya mwili – kwa sababu gani?
1 Wakorintho 5:4-5
“Katika jina la Bwana wetu Yesu, ninyi mkiwa mmekusanyika pamoja na roho yangu, pamoja na uweza wa Bwana wetu Yesu;
5 kumtolea Shetani mtu huyo, ili mwili uadhibiwe, ili na roho iokolewe katika siku ya Bwana Yesu.”
Na sasa je, tunajengaje juu ya wito wetu? Kwa mawe ya thamani na dhahabu, au kwa kuni, majani na mabua? (Tafadhali soma 1 Wakorintho 3:9-15).
1 Wakorintho 3:14-15
“Kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa, atapata thawabu.
15 Kazi ya mtu ikiteketea, atapata hasara; ila yeye mwenyewe ataokolewa; lakini ni kama kwa moto.”
- Baba yetu wa mbinguni hawezi kuwasha na kuzima upendo wake kwetu. Wengi wenu mlilelewa na baba – au pengine WEWE ulikuwa baba wa namna hiyo – ambaye aliwonyesha watoto wake upendo kwa masharti ya tabia njema. Lakini upendo wa Baba yetu wa mbinguni SI WA MASHARTI.
Tunaambiwa kuwa Mungu alitupenda hata tulipokuwa bado wabaya (“BADO wenye dhambi” – Warumi 5:6-9). Hili linawahusu ninyi Waislamu, Wahindu, Wayahudi, Wabudha, na Wakristo wote. Hadithi ya mwana mpotevu katika Luka 15 inaeleza jinsi huyu mwana mbaya kabisa alivyorudi kwa upendo wa furaha wa Baba yake!
Hivyo sasa, unapoendelea kufanya dhambi – kuanguka hapa na pale, si kama mtindo wa maisha – Mungu bado anakupenda na anakukubali. Inawezekanaje hilo? Kwa sababu wewe, “wewe wa zamani, mtu wa kale” – umekufa, na umesulubiwa pamoja na Kristo (Wagalatia 2:20), kwa kuwa sasa tunaonekana kuwa sehemu ya mwili wa Kristo mwenyewe. Mwana wa Mungu anaishi ndani yetu ikiwa tumemwamini.
Waefeso 1:5-6
“Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake;
6 Na usifiwe utukufu wa NEEMA Yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa.”
1 Yohana 2:3-6
“Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake. 4 Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake.
5 Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli. Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake.
6 Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda.”
- Hata tunapotanga-tanga, Mchungaji Mwema hutufuata! Na anapokupata, pengine umekwama kwenye miiba, anashangilia na anafanya sherehe anaporudi pamoja nawe. Mathayo 18:12-14. Baba ana nia ya kutopoteza hata mmoja wa watoto wake wadogo (mst wa 14).
Mtazamo wetu lazima uwe kwa Mwokozi wetu. Tunapokaa ndani yake, tunazaa matunda mengi (Yohana 15:5-6,8) na tunapomtazama YEYE, SIO sisi wenyewe, amini usiamini, tunazidi kufanana kama YEYE.
2 Wakorintho 3:17-18
“Basi “Bwana” ndiye Roho; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru.
18 Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho.”
Hapa ndipo tunapopaswa kuamini: kuwa na imani kwamba Mungu na Yesu wanasema kweli katika aya hizi zote. Yesu alilipa deni na akafa, Yesu alichukua ghadhabu ya Mungu juu yake kwa ajili yetu, na YEYE alihukumiwa kwa ajili yetu – mwenye hatia kwa sababu ya dhambi ZETU zilizowekwa juu yake – na akafa! “Mtu wetu wa zamani” – nafsi ya kale – alisulubiwa au alikufa pamoja na Kristo, Ndani ya Kristo, kulingana na Wagalatia 2:20.
Lakini bado tunao mwili wa asili, lakini Mungu hatuoni tena kuwa “katika mwili” – Warumi 8:9 – bali katika roho! Hivyo mwili unapofanya dhambi, ni “si mimi tena ninaetenda hayo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu” – Warumi 7:14-20. Mungu hukuoni wewe na mimi kama “katika mwili, bali katika roho.” Tunapaswa kuamini hivyo.
Tuna hukumu inayokuja kuhusu kile kitakachokuwa THAWABU yetu, lakini hukumu ya uzima wa milele IMEKWISHA, milele! Hakuna “hukumu mara mbili” kwa Mungu! Tumeshahukumiwa kuwa HATUNA DHAMBI tulipokuja kwa Mungu kupitia Kristo – kwa kuwa DHAMBI ZETU ZOTE ziliwekwa juu ya Yeshua! Na damu yake INAENDELEA kutusafisha dhambi zetu (1 Yohana 1:7).
Dhambi yetu ya kesho au ya mwezi ujao haitabadilisha UPENDO HUO WA NDANI tulio nao kutoka na kwa Mungu, alimradi anatuona tukijitahidi kupambana na dhambi, ingawa wakati mwingine tunashindwa. Mradi tunatubu kila mara pia. Lazima Uondoe kabisa mawazo kwamba Mungu ana upendo wa masharti, hasa katika Agano Jipya. Tena, soma Warumi 5. (Ninatambua kwamba katika Agano la Kale walikuwa na uwezo wa kuchagua uzima au mauti, baraka za kimwili zikiwa zimefungwa na utii.)
Lakini sasa kama watoto wa Mungu, tunapotubu, ni ili kurudishwa karibu tena – kwa kuwa tulikuwa tumepotoka kidogo kutoka njia sahihi – lakini DENI letu la kufa kwa ajili ya dhambi zetu limeshalipwa milele. Usiogope tena mauti ya pili.
Wengine wenu mnapambana sana na jambo hili… Ninahisi kabisa jambo hili rohoni mwangu! Shetani anataka kuwatawala kwa HOFU kwamba “hamtafanikiwa”! Mkemeeni Shetani! Mawazo hayo ni yake, si yenu. MWAMBIE kwamba Mwokozi wako tayari ameshafanikiwa kwa ajili yako. Umepewa uzima wa milele na unapaswa kujua hilo. Umezaliwa upya ndani ya familia ya Mungu na wewe ni wa Mungu. Na hakuna kitu—fahamu hili—HAKUNA kitu kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu (Warumi 8:38-39).
Je, unaamini maneno ya Yeshua? Au huna imani nayo?
Yohana 5:24
“Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka YUNA uzima wa milele, wala haingii hukumuni, bali AMEPITA kutoka mautini kuingia uzimani.”
Je, FURAHA ya wokovu wako iko wapi?
Mfalme Daudi alifanya mfululizo wa dhambi za kutisha alipompanga mmoja wa askari wake bora apokonywe mke wake wa pekee na kisha akamfanya mjamzito! Halafu akapanga Uria auawe vitani. Mungu alikasirika sana kwa jambo hilo na kulikuwa na matokeo mengi yaliyoahidiwa na Mungu – lakini BADO, Daudi alizungumza kuhusu kurejeshwa tena kwa FURAHA ya wokovu wa Mungu. Na katika sala ile ile alitoka kwenye shimo la huzuni na toba akaingia katika FURAHA ya wokovu (Zaburi 51:12)
Lakini inaonekana wengi wenu mnaokuja kwa Kristo, au ambao tayari mpo ndani ya Kristo, hamna furaha ya wokovu au mna kiasi kidogo sana cha furaha hiyo kwa sababu hamuamini hili!
Makundi ya “Makanisa ya Mungu”: Wanaamini kuwa WAO ndio wataweza “kuingia” katika Ufalme, au kupata wokovu – na hivyo wanakana imani yao katika Yeshua ambaye tayari ameshafanikiwa na ametimiza mahitaji yote kwa ajili yetu (Warumi 8:1-4). Lakini kwa kuwa wanashindwa kuishi maisha ya ukamilifu, wanakuwa mabingwa wa hatia. Basi ACHA kuhisi vibaya kila wakati. Una Mwokozi! Umepita kutoka mauti kwenda uzima.
LAKINI, hatutaki pia kuwa wazembe, watu wa kiburi au waasherati wa kiroho kama Laodikia (Yuda 4, Ufunuo 3)! Tunataka kuwa watu wa bidii, tukijitahidi kupambana na dhambi – na hilo litatokea zaidi na zaidi kwa kukaa ndani ya Kristo na kumtazama YEYE.
Wakatoliki – KOMA! Hamuhitaji kufanya toba ya kujitesa.
Wabudha na Wahindu – KOMA! Kwa Mungu wa kweli hamuhitaji kuogopa kwamba mtaishi tena kama ng’ombe au MDUDU kwa sababu hamkuwa wakamilifu katika maisha haya.
Waislamu: Mnaweza kuwa na uhakika, katika dini ya kweli ya Mungu, kwamba mna maisha ya baadaye yaliyo na mwangaza, badala ya kuwa na shaka kama Allah atawapa uzima wa milele Peponi au la! Hamuhitaji kuwa na wasiwasi kama mema yenu yatashinda mabaya yenu. Njoo kwenye furaha ya kweli, amani, na ujue kwamba unaweza kuwa na uzima wa milele.
Kumbuka kwamba maisha ya Yeshua, ambaye alikuwa NENO pamoja na Mungu, yalikuwa ya thamani zaidi kuliko maisha ya binadamu wote waliowahi kuzaliwa, kwa hiyo maisha yake moja yalilipia dhambi za wote WANAOKUBALI neema ya Mungu. Najua kwamba Quran inasema hakuna anayeweza kulipia dhambi za mwingine. Lakini katika kweli ya Mungu wa kweli, maisha ya Yeshua YANAWEZA kukufia na kukuokoa – lakini ni lazima umkubali kwa unyenyekevu.
Tamka waziwazi imani yako kwake na umwamini Yesu – na upokee zawadi yake ya bure ya msamaha wa dhambi zote na kukupa kibali, neema, baraka, kukubaliwa – na uzima wa milele. Zawadi ya Mungu SI kitu tunachoweza kuilipia, kuistahili au kuifanyia kazi (Waebrania 11:5-6). Mungu anatupenda, anatupa kibali chake na baraka zake ingawa hakuna hata mmoja wetu anayestahili. (Warumi 5:17 – kipawa cha haki)
Njoo uamini kweli kwa FURAHA ya ndani maandiko yanayosema wazi kwamba sasa hivi tunao uzima wa milele na wokovu ikiwa tutavumilia na tusimkane Mungu milele katika maisha yetu. Wengine walinipinga niliposema TUNA uzima wa milele sasa, lakini nina uhakika kwamba ninaweza kuamini Neno la Mungu!
1 Yohana 5:11-13
“Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu ALITUPA uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe.
12 Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima.
13 Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili MJUE ya kuwa mnao uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu.
Kuna maandiko MENGI yanayotuambia kwamba kwa kumwamini Yeshua, tumehamishwa kutoka mauti kwenda uzima na sasa hivi tunao uzima wa milele, kwa jinsi Mungu anavyoona. Hata yale maovu uliyoyafanya yamesamehewa katika Kristo. Lakini kama hutamruhusu Kristo kufuta dhambi zako ndani yake, basi bado uko chini ya ghadhabu ya Mungu (Yohana 3:36). Lakini ukikiri imani yako kwa Yeshua, umepita kutoka katika mauti uliyoistahili – kwenda kwenye ZAWADI YA BURE ya Mungu, neema yake ya ajabu isiyoelezeka.
LAZIMA TUSHIRIKISHE NA KUPANUA NEEMA kwa watu wote.
Sasa hebu tuingie sehemu nyingine kidogo. Tayari umepokea kibali cha Mungu na upendo wake. Sasa tufanye nini? Baba yetu na Mwokozi wetu hawataki tukifiche kibali hicho ndani yetu. Tunapaswa KUSHIRIKI na KUKUA katika neema ya Bwana na Mwokozi wetu (2 Petro 3:18)
Kwanza kabisa, uko katika mwili wa Kristo ikiwa unayo Roho wake (Warumi 8:9, 14). Na tunapaswa kuwaona kila mmoja wetu kama TUNAHUSIANA, kama watu wanaomilika kila mmoja kwa mwenzake. Sisi ni kama viungo vya mwili mmoja—vyote vimeunganishwa kufanya kazi.
Warumi 12:5
“vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake.”
Unapomhukumu ndugu mwingine aliye sehemu ya mwili wa Kristo, si rahisi kumwona Yeshua akifurahia jambo hilo! Tazama Warumi 14:10. Zaidi ya hapo, tutahukumiwa kwa kipimo tulichotumia kwa ndugu zetu. Mungu anataka tuwaheshimu na kuwathamini wenzetu—hata ZAIDI ya sisi wenyewe (Wafilipi 2:3)
Chochote Mungu anachotufanyia, katika sisi, kwa ajili yetu, au kwetu—anataka tukishirikishe kwa wengine. Na tunapoonyesha neema yake kwa wengine, tunapokea zaidi. Heri wenye rehema, maana hao watapata rehema (Mathayo 5:7).
Wakolosai 4:6
“Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu.”
1 Petro 4:10
“Kila mmoja kwa kadiri alivyoipokea KARAMA, ITUMIENI kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu.”
Ikiwa unamwona ndugu ana uhitaji, lakini unaufunga moyo wako usimsaidie, unaweza vipi kusema kwamba unampenda Mungu? Hili limetajwa mara nyingi katika 1 Yohana. Mungu anapotufariji sisi, tunapaswa kutumia faraja hiyo hiyo kuwafariji wengine (2 Wakorintho 1:3-4).
Sasa fikiria kuhusu neema ya Mungu, kibali chake, msamaha wake, kukukubali pamoja na dhambi zako zote. Je, unaweza sasa kupitisha huo msamaha, kukubali, na rehema kwa familia yako ya Mungu? Umesamehewa mara MINGI (Mathayo 18:21-35 – soma).
Je, huwezi kumsamehe ndugu yako kwa kile ulichosikia kupitia umbea? Je, wewe mwenyewe hukutenda dhambi kwa kusikiliza umbea huo na kisha ukautumia kumhalalishia moyo wako mgumu dhidi ya ndugu yako katika Kristo? Kwa maana tusiposamehe na kukubali kila mmoja, nasi hatutasamehewa. (Mathayo 18:35)
Mathayo 18:32-35
“Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi; 33 nawe, je! Haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? 34 Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote.
35 “Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu Ndugu yake.”
Hili limenitokea mara nyingi (si kusamehewa) na imelazimu kumuomba Mungu awasamehe kwa ugumu wa mioyo yao na anisaidie mimi mwenyewe nisiwe na moyo kama huo.
Hadithi ya Binti yangu – wakati wa ibada kanisani, nilikuwa nahubiri, na binti yangu mwenye umri wa miaka 9 alikuwa hatulii wala haheshimu ibada. Nilikuwa tayari kumrudi. Nilikuwa tu nimetoa mahubiri kuhusu moyo wa Mungu uliojaa rehema. Akainama chini, akasema, “Baba, unaweza kunionyesha rehema na kunipenda kama Mungu anavyofanya?”
Bila shaka ilibidi niwe na neema na rehema kwake wakati huo!
Watu wanapaswa kujifunza zaidi kuhusu Mungu, upendo wake, neema yake, na jinsi anavyokubali, KUPITIA na kwa sababu ya yale wanayaona katika maisha ya watoto wake wale wanaowapa kibali hata wale waliokuwa wauaji, wabakaji, wadhulumu wa watoto, magaidi wakati wanapotubu na kumrudia Mungu. Nimetaja dhambi hizi ambazo watu huchukulia kuwa mbaya zaidi ili kufikisha hoja yangu. Lakini dhambi zako na zangu ndizo zilizosababisha Yesu asiye na hatia kufa msalabani. Dhambi zangu pia zilisababisha. Sote tumesababisha kifo kile kile, kwa hiyo … tusikatae kuwasamehe waliokuwa walevi, wazinzi, au lolote walilokuwa zamani.
Kumbuka simulizi la 1 Wakorintho 5 kuhusu yule mwenye dhambi ya uasherati aliyefukuzwa kwenye ushirika? Lakini baada ya muda, Paulo aliwaambia Wakorintho wampokee tena kwa UPENDO mtu huyo aliyekuwa mbaya sana, lakini sasa amesafishwa, sasa mpokeeni.
2 Wakorintho 2:5-9
“Lakini iwapo mtu amehuzunisha, hakunihuzunisha mimi tu, bali kwa sehemu, (nisije nikalemea mno), amewahuzunisha ninyi nyote. 6 Yamtosha mtu wa namna hii adhabu ile aliyopewa na walio wengi.
7 hata kinyume cha hayo, ni afadhali zaidi mmsamehe na kumfariji, mtu kama huyo asije akamezwa katika huzuni yake ipitayo kiasi.
8 Kwa hiyo nawasihi kumthibitishia UPENDO wenu. … 2:11 -- Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake.”
Kisha katika 2 Wakorintho 5:17, Paulo anasema sisi ni “kiumbe kipya” katika Mungu. Na katika mistari ya kabla ya hapo, Paulo anasema “Acheni kuwaza kuhusu wengine kwa jinsi WALIVYOKUWA ZAMANI kabla ya kuitikia mwito wa Mungu wa uzima wa milele.”
Hilo linajumuisha kuacha kusengenya au kusikiliza umbea kuhusu dhambi za wengine. Upendo wa Mungu na neema yake hufunika wingi wa dhambi! Na sisi tunapaswa kufanya vivyo hivyo.
Narudia tena, inakuwa rahisi zaidi kuamini kwamba MUNGU amekusamehe, pale unapoona upendo wa kweli, msamaha na kukubalika KWAKO, na dhambi zako zilizooshwa - kutoka kwa ndugu zako katika Kristo.
Usiwe kama kaka mkubwa wa mwana mpotevu. Tafadhali usiwe hivyo! Karibisha kwa upendo na kwa furaha wale ndugu waliokuwa wenye dhambi sana lakini sasa wamerudi kwa Baba! Waache wamsifu Mungu pamoja nawe.
Natumaini mahubiri haya yamekupa jambo la kufikiria kwa kina. Shiriki neema ya Mungu.
MAMBO YA KUKUMBUKA KUHUSU NEEMA NA KIBALI CHA MUNGU:
- Mkusudi wa Neema ya Mungu ni kufungua njia kwa mtu ye yote ulimwenguni ambaye Mungu anamwita awe sehemu ya FAMILIA YAKE ya watoto. Yeshua ni Mwokozi wa ULIMWENGU.
- Tunaishi katika FURAHA ya neema ya Mungu, tukitambua kwamba sisi ni watoto wake WAPENDWA, tunampendeza, na tumekubaliwa katika Kristo (Yohana 17:23)
- Tunayaelekeza macho yetu zaidi kwenye kile Kristo anachotufanyia ndani yetu kuliko kile tunachofanya sisi wenyewe (Waebrania 12:2; 2 Wakorintho 3:17-18). Hivyo tunakua kufanana na Kristo kwa utukufu wa Mungu.
- Lazima TUSHIRIKISHE zawadi ya neema/kukubaliwa na Mungu kwa wengine—bila kujali walikuwa waovu kiasi gani kabla. Sisi pia tuwakubali. Kristo -- rafiki wa wenye dhambi. Ndivyo nasi tunavyopaswa kuwa. Hii ni sehemu ya injili ya neema ya Mungu (Matendo 20:24)
- Tunaokolewa (kumesamehewa, kupewa uzima wa milele) BURE kwa neema kama karama ya Mungu ambyo hatuwezi kuilipia wala kuifanyia kazi; lakini tunalipwa thawabu kwa matendo yetu mema (thawabu = tutakavyokuwa na tutakavyofanya milele) (Waefeso 2:8-10)
- DHAMBI ZETU ZOTE zimesafishwa milele, na kwa Mungu zimepuuzwa na kusahauliwa! (Waebrania 8:12; 10:17). Pia tunapaswa kuacha kuangalia nyuma.
- Tunamkiri Kristo na kuamini kuwa yu hai, tunatubu, tunabatizwa, tunapokea Roho wa Mungu, sasa tunakuwa mali ya Kristo kwa neema kuu ya Mungu, hivyo basi:
- Sasa UNAMILIKIWA na Mungu. Tumezaliwa katika familia yake. Hatujijisimamii tena. Yeye ndiye mwenye mamlaka juu yetu. Kusudi kuu la Neema lilikuwa ni kuweka njia ya kumpatia Mungu familia takatifu na yenye haki.
- Sasa unapofanya dhambi, HUKUMIWI tena
(Warumi 8:1; Yohana 3:17-18), lakini Mungu anaendelea kutupenda, kama baba alivyompenda mwana mpotevu. - Hatupotezi Roho wa Mungu sasa isipokuwa tukiamua sisi wenyewe kumwacha milele. Roho Mtakatifu wa Mungu ni muhuri wa wokovu wetu.
(Waefeso 1:13-14). - Mungu hatutengi naye tunapotenda dhambi sasa, ingawa lazima tutubu. Hatatuacha wala hatatupungukia kamwe (Waebrania 13:5). Hakuna kitu kinachoweza kututenga na upendo wa Mungu. Romans 8:31-39.
- Kifo cha Kristo kilifunika na kulipa DENI la dhambi zetu zote, mara moja kwa wakati wote. (1 Yohana 1:9). Deni ya mauti imelipwa mara moja tu, kwa nyakati zote kwa ajili yako. Hii inakuweka huru kutoka kwa utawala wa Shetani. Sasa uko huru.
- Damu yake inaendelea kutusafisha (kitendo kinachoendelea) tunapotenda dhambi au kujikwaa katika dhambi baada ya kuwa watoto wa Mungu -- 1 Yohana 1:7; 1 Yohana 5:11-13).
- Tumetoka mautini na kuingia uzimani na tunaonekana kuwa na uzima wa milele sasa. Yohana 5:24 Hatuhitaji kuogopa kifo cha pili au kujiuliza kama “tutafanikiwa” kuingia katika ufalme wa Mungu. Tayari tumefuzu (Wakolosai 1:12; Warumi 8:2-4).
- Sadaka ya Kristo mara moja kwa wakati wote imekufanya kuwa mkamilifu WEWE na wote wanaotakaswa.
(soma Waebrania 10:14). (Hayo yote yalielezwa katika mahubiri yangu ya “Ukamilifu”)
Kuanzia sasa tunapaswa kuishi katika maisha ya utukufu ya neema na kibali cha Mungu, tukipendwa, na kukubalika na Yeye, ndiyo – hata tunapoteleza—kwa kuwa Yeye atahakikisha anaturudisha katika Njia sahihi. Anatuhakikishia hiyo. Wokovu ni kazi YAKE pekee, kumbuka. Ni wokovu kwa neema, si kwa matendo, kwa utukufu wake.
Tumalizie na kifungu hiki:
Waebrania 9:27-28
“Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu;
28 kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, PASIPO DHAMBI, kwa hao WAMTAZAMIAO kwa WOKOVU.”
Maombi ya kufunga